HALMASHAURI
YA WILAYA YA MASWA
OFISI
YA MBUNGE - JIMBO LA MASWA MAGHARIBI
MKOA
WA SIMIYU.
TAARIFA
YA UTEKELEZAJI WA
ILANI
YA CHAMA CHA MAPINDUZI
KATIKA
JIMBO LA MASWA MAGHARIBI,
2015/2016
- 2019/2020.
1.
ELIMU.
Katika
kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa sekta ya elimu, Jimbo ilijiwekea
malengo ya kuhakikisha kuwa vijiji vyote vilivyoko jimboni vinakuwa na shule ya
msingi ili kuhakikisha kuwa watoto wote waliofikisha umri wa kwenda shule
wanaandikishwa. Lengo linguine lilikuwa kuhakikisha kwamba kata zote zinakuwa
na shule ya sekondari ili kuwezesha watoto wote wanaofaulu wanajiunga na masomo
ya sekondari.
Inaendelea ...........
Inaendelea ...........
Utekelezaji:
Elimu
ya Msingi. Mbunge alishiriki kikamilifu katika
uhamasishaji wananchi kuchangia nguvu, muda na raslimali pesa ili kujenga
madarasa katika vijiji 3 vya Ngazu, Mwakulilima na Ng’hungu. Hivi ni vijiji vilivyokuwa
havina shule za msingi kabisa. Watoto walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda
kwenye shule zilizoko vijiji vingine. Jumla ya madarasa 8 yamejengwa, madarasa
4 kila kijiji yamejengwa na shule kufunguliwa katika kijiji cha Ngazu na kijiji
cha Mwakulilima. Madarasa 2 na ofisi ya mwalimu yamekwisha kujengwa katika kijiji
cha Ng’hungu na shule itafunguliwa baada ya choo cha shule kukamilika.
Mwonekano wa baadhi ya madarasa ya shule ya msingi Ngazu.
Kwa
sababu ya ongezeko la watoto walioandikishwa kujiunga na madarasa ya awali na
shule za msingi mwaka 2016, na kwa kuwa utekelezaji wa sera ya elimu bila
malipo sera inayotekelezwa na serikali ya awamu ya tano ulihamasisha wazazi
kuwapeleka watotowao shuleni, uandikishaji katika shule za msingi uliongezeka
Zaidi na matokeo yake watoto wengi walikosa madarasa ya kusomea. Kwa
kushirikiana na halmashauri ya wilaya, mbunge alihamasisha ujengaji wa madarasa
jimboni ambapo kila kijiji kiliweza kujenga boma moja la darasa na mbunge
kupitia mfuko wa jimbo alitoa bati 40 kila shule ya msingi ili kuezeka madarasa
hayo. Jumla ya madarasa 58 yaliezekwa kupitia mpango huo kwa maana ya darasa
moja kila kijiji chenye shule ya msingi.
Ili
kuhakikisha miundo mbinu ya shule inatosheleza mahitaji ya wanafunzi, mbunge
alitoa kutoka mfukoni mwake pesa yenye kutosheleza mbao zenye kutosheleza
kuezeka madarasa 3 na ofisi 1 (Thamani ya Tshs 3,388,000/=) katika shule ya
msingi ya kijiji cha Zawa. Shule hii ina wanafunzi wa darasa la kwanza mpaka
darasa la saba, lakini ilikuwa na vyumba 4 tu vya madarasa, hivyo kulazimika
wanafunzi wa madarasa mengine kusomea darasa moja kwa mtindo wa mzungu wa nne (mzungu
four).
Katika
kuhamasisha na kuwatia hamasa walimu wa shule za msingi walioshika namba kumi
bora katika wilaya kwa matokeo ya mitihani ya darasa la saba mwaka 2016, mbunge
alitembelea shule zote kumi zilizofanya vizuri na kuwapa zawadi ya mipira 2 (wa
miguu na pete) kila shule na kuwapatia walimu Tshs laki moja (100,000/=) kwa kila shule iliyofanya vizuri kama motisha
kwa walimu kwa kusaidia watoto kufanya vizuri katika masomo yao. Mpango huu wa
kuhamasisha walimu kufundisha kwa bidi unaendelea ambapo mheshimiwa mbunge aliahidi
na kutoa Tshs 50,000 kwa kila mwalimu wa sekondari ambaye somo lake litapata A
katika mtihani wa taifa kwa mwaka 2018. Pia mbunge ameahidi kuwapatia Tshs laki moja
kila shule ya msingi itakayokuwa miongoni mwa shule kumi bora ki wilaya.
Zawadi ya mipira na jezi kwa shule
ya msingi Igwata ilikuwa miongoni mwa shule kumi bora kiwilaya.
Kwa
upande wa elimu ya sekondari, tumewezesha kwa mara ya
kwanza katika jimbo, kuwa na sekondari
ya kidato cha tano na sita (Malampaka High School) kuanzia mwaka 2016.
Tulifanya mawasiliano na wizara ya elimu kupitia waziri wa elimu profesa
Ndalichako na kukubali kutupatia pesa ili kujenga bwalo la chakula, kujenga
mabweni 2, kumalizia mabweni 2 yaliyokuwa hayakukamilika, kuweka umeme, na
kuchimba kisima cha maji. Sasa hivi tayari shule ina kidato cha tano na sita.
Ili
kuwasaidia watoto wa kike kuwaepusha na kutembea umbali mrefu, tumejenga bweni
moja la kukaa wasichana katika shule ya Sekondari Badi na kusaidia gharama za
uwekaji wa umeme shuleni hapo. Ofisi ya mbunge ilitoa wazo la kuanza ujenzi wa
bweni na kuchangia mifuko 200 ya simenti ili kuanza ujenzi. Wananchi wa kata ya
Badi walitoa mchanga, mawe na fedha kwa ajili ya kumlipa fundi ili kujenga
boma. Baada ya hapo mbunge aliwaomba Shirika lisilo la kiserikali la World
Vision kusaidia upauaji na kumalizia hatua zote zilizokuwa zimebaki. Ombi hilo
lilikubaliwa. Kwa niaba ya wananchi tunawashukuru sana Shirika la World Vision
kwani wamekuwa waungaji mkono wakubwa kwa maendeleo ya jimbo. Bwalo
limekamilika na linatumika kwa sasa.
Mbunge
(Mashimba Ndaki) akishiriki ujenzi wa bweni la wasichana – Badi sekondari.
Kwa
kusaidiana na benki ya NMB tumewezesha kuezeka madarasa 2 na ofisi shule ya
sekondari Mataba. NMB walitoa mabati na mbunge akatoa simenti mifuko 100 ya
kumalizia kuweka lenta, kupiga lipu na kununua mbao zote za kuezekea. Jumla ya
gharama zilizotolewa na mbunge ni Tshs ……..kutoka katika mfuko wa jimbo.
Kati
ya kata 17 zilizoko kwenye jimbo la Maswa Magharibi, Kata 2 hazina sekondari za
kata, nazo ni kata za Zanzui na kata ya
Mwang’honoli. Mbunge kwa kushirikiana na wananchi wa kata hizo wameanzisha
ujenzi wa shule za sekondari na mpaka sasa hivi kuna maboma ya madarsa manne na
ofisi 2 katika kata ya Zanzui. Madarasa 2 na ofisi 1 tayari yameezekwa. Mbunge
alitoa mabati 240 yenye thamani ya Tshs 6,000,000 kutoka mfuko wa jimbo. Katika
kata ya Mwang’honoli tayari madarasa 2 na ofisi yameshajengwa na kuezekwa.
Mbunge alitoa fedha za mfuko wa jimbo Tshs 1,495,000 ili kusaidia uezekaji.
Katika
juhudi za kutaka kuwa na makazi bora kwa walimu wa shule za sekondari, serikali
ilitoa Tshs 150,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 6 za walimu shule ya
sekondari ya Mwabayanda. Hii ilikuwa ni juhudi za mbunge baada ya kuzungumza na
uongozi wa wizara ya elimu juu ya umuhimu wa shule hii kuwa na makazi ya walimu
kwa kuwa iko maeneo ya pembezoni sana.
Elimu
ya ufundi ni muhimu sana hasa wakati huu ambapo vijana wengi wanamaliza darasa
la saba na sekondari lakini hawachaguliwi kuendelea na masomo ya elimu ya juu. Kwa kulitambua hilo mbunge kwa
kushirikiana na halmashauri ya wilaya walipeleka maombi ya kuboresha chuo cha
maendeleo ya wananchi Malampaka na serikali imetoa fedha kiasi cha Tshs 590,000,000
ili kujenga majengo mapya ikiwemo mabwalo ya wasichana na wavulana, kuongeza
madarasa na kujenga karakana moja. Baada ya kukamilika uboreshaji huu, chuo
kitakuwa na uwezo wa kudahiri wanafunzi wengi Zaidi na hivyo kusaidia vijana
wengi kupata ujuzi ili wajiajiri wenyewe.
Ufaulu
mkubwa wa wanafunzi wa darasa la saba mwaka 2018 ulisababisha miundo mbinu ya
madarasa katika shule za sekondari kuzidiwa na kusababisha baadhi ya wananfunzi
waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2019 wasianze masomo kwa sababu
ya upungufu mkubwa wa vyumba vya kusomea. Mbunge kwa kusaidiana na halmashauri
ya wilaya alihamasisha wananchi katika jimbo kujenga na kumaliza boma la darasa
moja kila shule ya sekondari katika sekondari zote 17 zilizoko jimboni. Katika
jitihada hizo serikali ilitoa Tshs 150,000,000 ili kuunga mkono juhudi za
wananchi katika kuhakikisha kuwa madarasa yaliyopungua yanakamilika na kuanza
kutumika ili watoto waliochaguliwa lakini hawakujiunga na kidato cha kwanza kwa
sababu ya upungufu wa madarasa waende shule. Shule za sekondari 7 zilipata
msaada huo wa serikali.
Ili
kuwezesha kuinua taaluma katika shule zetu, ofisi ya mbunge kupitia mfuko wa
jimbo iiwezesha upatikanaji wa mashine ya kudurufu mitihani (photocopier
machine). Mashine hii imesaidia kudurufu mitihani ya wilaya na kimkoa na
kurahisisha ufanyaji wa mitihani kwa wanafunzi.
2.
AFYA:
Ili
kutekeleza Ilani ya CCM jimboni kwa upande wa sekta ya afya, lengo kuu lilikuwa
kuboresha huduma za afya jimboni kwa wananchi wote hususani wanawake na watoto.
Utekelezaji:
Uboreshaji wa kituo cha afya Malampaka
umekamilika. Serikali ilitoa milioni 500 ili kukiboresha kituo hiki na kazi
zifuatazo zimekamilika: Jengo la upasuaji limekamilika. Jengo la wodi ya
kawaida limekamilika. Chumba cha maabara kimekamilika. Jengo la nyumba ya
mtumishi limekamilika. Jengo la kuhifadhia maiti nalo limekamilika. Kukamilika
kwa uboreshaji wa kituo hiki utapunguza kwa kiasi kikubwa vifo vinavyotokana na
uzazi kwa wanawake lakini pia kupata huduma za upasuaji karibu badala ya
kusafiri umbali mrefu.
Mbunge (wa tatu kutoka kulia) akiwa
na baadhi ya viongozi na wananchi walipotembelea kituo cha afya Malampaka.
Ujenzi wa kituo cha afya cha Mwabayanda
unaendelea vizuri. Hii ni baada ya serikali kutoa kiasi cha Tshs milioni 400. Majengo
yanayoendelea kujengwa katika kituo hiki cha afya ni pamoja na jingo la wodi ya
akina mama, jingo la upasuaji, jingo la maabara, nyumba ya mtumishi, jingo la
maabara na jingo la kuhifadhia maiti. Kituo hiki kitakapokamilika kitahudumia
wananchi wa kata za Mwabayanda, mwang’honoli, Kulimi na baadhi ya vijiji vya
kata ya Busangi na Nyabubinza.
Ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Mwabayanda
uko katika hatua za mwisho kukamilika.
Katika azima ya kuwasaidia akina mama jimbo
pia lilipata ufadhili wa shirika la AMREF kwa kujenga wodi za akina mama katika
zahanati za Masela, Mwabagalu, na Jija. Pamoja na wodi hizo, shirika pia
linasaidia kujenga vituo vya kuelimisha vijana katika zahanati hizo ili vijana
wawe wanaelimishwa kuhusu mambo yanayohusu uzazi salama. Wodi nyingine ya
wazazi iliyojengwa ni ile ya zahanati ya Badi ambapo serikali kwa kushirikiana
na UNFPA wamewezesha kukamilika kwa jingo hilo.
Kwa kutumia mfuko wa jimbo na michango ya
wananchi, mbunge amewezesha kuezekwa kwa maboma 8 ya zahanati katika vijiji vya
Kizungu, Mwang’anda, Mwatumbe, Nyabubinza, Bukangilija, Jihu, Isulilo na Wigelekelo. Mbunge kwa
kushirikiana na Halmashauri ya wilaya aliomba Shirika la World Vision kumalizia
zahanati za Mwatumbe na Wigelekelo, Shirika hilo lilikubali na tayari
linamalizia ujenzi wa zahanati hizo 2. Mbunge pia amepeleka maombi kwa shirika
hilo ili kumalizia zahanati za Mwang’anda na Jihu mwaka ujao wa fedha.
Kwa msukumo wa mbunge pia kupitia mfuko wa
jimbo, serikali kwa kusaidiana na wananchi tumewezesha kumalizia ujenzi wa
zahanati ya kijiji cha Kidabu, zahanati iliyojengwa boma lake muda mrefu lakini
haikukamilika. Sasa hivi wananchi tayari wanapata huduma kwenye zahanati hii
baada ya kuimalizia. Kwa mtindo huo huo wa kusaidiana na wananchi, mbunge na
serikali, tumeweza kujenga jengo la wagonjwa katika zahanati ya kijiji cha
Igunya na tayari jengo hilo lilishakamilika na linatumika.
Kwa kutumia mfuko binafsi na kushirikisha
wadau mbalimbali wa maendeleo mbunge, aliweza kutoa magodoro 10 kwenye kituo
cha afya cha Malampaka na kutoa vifaa vya kutumia wakati mama anajifungua na
baada ya kujifungua (birthing kits) kwa zahanati za Badi, Masela, Seng’wa na
kituo cha afya cha Mwasayi. Aidha, ofisi ya mbunge ilichangia kwa sehemu kubwa
kupitia mfuko binafsi wa mbunge ujenzi wa vyoo vya wanafunzi vya shule ya msing
Sayusayu, shule za sekondari Mataba, na Mwabayanda.
3.
MAJI
Lengo kuu katika sekta hii ya maji
lilikuwa kuwapatia maji safi na salama wananchi wa jimbo la Maswa Magharibi na
kuhakikisha kwamba akina wametua ndoo kichwani.
Utekelezaji:
Mradi mkubwa wa maji umeanzishwa Kata ya
Mwang’honoli. Mradi huu uko katika vijiji viwili vya Mwabulimbu na Ngazu. Hatua
iliyofikiwa ni uwekaji wa mashine ya kusukuma maji, ulazaji wa mabomba na
ujenzi wa vituo vya kuchotea maji (water points). Kwa sasa mradi uko katika
hatua za mwisho za majaribio kupeleka maji katika vijiji vya Mwabulimbu na
Ngazu. Mradi huu ni matokeo ya juhudi za mbunge wa jimbo kufuatilia upatikanaji
wa fedha kwani kisima kinachotumika kutoa maji kilichimbwa zamani lakini fedha
za ujenzi wa mtandao wa maji ikiwa ni pamoja na kuweka mashine ya kusukuma maji
hazikupatikana. Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya tano chini ya Mheshimiwa
Rais John Pombe Magufuli kwa kutupatia fedha taslimu kiasi cha Tshs milioni 500
za kukamilisha mradi huu.
Katika kata ya Badi kuna miradi miwili ya
maji ya kupeleka maji katika vijiji vya Jihu, Ikungu, Nyashimba na Muhida.. Mradi
huu utakuwa na mashine 2 za kusukuma maji, moja itasukuma maji kupeleka vijiji
vya Jihu na Ikungu na nyingine itasukuma maji kupeleka vijiji vya Nyashimba na
Muhida. Mpaka sasa hivi majengo ya pampu yote mawili yameshakamilika, ulazaji
wa mabomba kwenda vijiji vya Jihu na Ikungu umekamilika, vituo vya kuchotea
maji vyote vimeshajengwa na ujenzi wa matanki unaendelea vizuri. Mradi utakapokamilika
utawasaidia wananchi wa vijiji vinne kuwa na maji safi na salama.
Kwa kushirikiana na shirika la World
Vision, mradi wa kisima kirefu ulichimbwa katika kijiji cha Isulilo na
kuwezesha kupatikana maji mengi ya kutosheleza wakazi wa kijiji hicho.
Mheshimiwa mbunge amewaomba Shirika hilo kusaidia kuweka mashine ya kusukuma
maji ili maji ya kisima kilichochimbwa yaweze kuwafikia watu wengi. Shirika
limekubali na kazi ya kuchimba mitaro inaendelea kufanywa na wananchi. Mradi
huu utakapokamilika utakuwa na vituo 6 vya kuchotea maji kwenye kila kitongoji
cha kijiji cha Isulilo.
Katika kata ya Jija, kabla ya kuchaguliwa
kuwa mbunge kulikuwa na mradi wa maji uliokuwa umekwama kwa muda wa miaka 3.
Mradi huu ulikosa ufuatiliaji hali iliyopelekea mradi kutokamilika kwa wakati.
Kwa ufuatiliaji wa mbunge, mradi ulitekelezwa na kukamilika mwaka 2017.
Mradi wa Sayusayu extension unaokusudia
kupeleka maji kijiji cha Ng’haya uko kwenye hatua nzuri ya kukamilika. Kazi ya
kujenga vituo vya kuchotea maji imekalika na ulazaji wa mabomba unaendelea
vizuri. Mradi utakapokamilika utawasaidia sana wananchi wa kijiji cha Ng’haya
kwa kuwa hupata maji kutoka umbali mrefu.
4. BARABARA/RELI NA UMEME:
Katika kipindi tajwa miundo mbinu ya
barabara na umeme imeimarishwa na mingine kujengwa upya. Wakati awamu ya tano
inaanza kulikuwa na vijiji 14 ambavyo havikuwa na umeme katika jimbo. Mpaka
wakati wa kuandika taarifa hii vijiji 4 tayari vimeshafikiwa na umeme wa REA,
ambavyo ni Inenwa, Nhelela, Gumali, na Kakola. Bado vijiji 10 havina umeme.
Kuhusu barabara, Jimbo limeweza
kufunguliwa kwa barabara zinazounganisha vijiji na vijiji. Barabara kutoka kijiji
cha Gulung’washi kata ya Malampaka kwenda Kata ya Kadoto kupitia Mwabulimbu,
Mwang’honoli, na Zawa imelimwa kwa kiwango cha changalawe. Barabara hii
itaiwezesha kata ya Kadoto na Mwang’honoli kupata huduma yake kwa urahisi
kutoka mji mdogo wa Malampaka na hivyo kuchagiza shughuli za kiuchumi za
wananchi wa maeneo hayo. Barabara ya kuunganisha kijiji cha Jihu na Ikungu imelimwa
ili kufanya kijiji cha Ikungu kuunganishwa na vijiji vya Muhida na Malampaka.
Barabara ya kutoka Kulimi kuunganisha vijiji vya Mwamihanza na Ngongwa
inafanyiwa matengenezo pia.
Kwa upande wa reli, tunaishukuru sana
serikali ya awamu ya tano chini ya Mheshimiwa Rais Dr. John Pombe Joseph
Magufuli kwa ujenzi wa reli ya kisasa. Reli hii inapita katika jimbo letu na
matarajio yetu ni kwamba mipango ya kujenga bandari kavu katika kituo cha
Malampaka itaendelea sambamba na ujenzi wa reli hiyo. Kwa upande wa jimbo
tayari tumeiomba halmashauri ya wilaya kupima viwanja katika mji mdogo wa
Malampaka na tayari wilaya imetekeleza hilo. Kwa sasa tayari kuna viwanja vya
kujenga maghala, makazi, nyumba za kulala wageni na mahotel. Tunaendelea
kuhamasisha wananchi wa ndani ya jimbo, wilaya, mkoa na kwingineko wajitokeze
kujenga ili reli itakapokamilika kila kitu kiwepo ikiwa ni pamoja na mahali pa
kuhifadhi bidhaa mbalimbali zitakazokuwa zikishushwa bandari kavu ya Malampaka.
Madaraja na vivuko mbalimbali yamejengwa
ikiwa ni pamoja na daraja la Kinamwigulu ambalo lilikuwa limekatika muda mrefu
na hivyo kusababisha vijiji vingi kutengwa na makao makuu ya wilaya. Sasa hivi
daraja hilo limekamilika na wananchi wanapita kwa urahisi wanapofanya shughuli
zao za kiuchumi. Barabara kuunganisha kata ya Zanzui na kata ya Mwamashimba
ilifanyiwa matengenezo na kuweka vivuko kati ya kijiji cha Zanzui na Dodoma
kuwezesha kupitika wakati wote wa mvua na masika.
Mheshimiwa mbunge anaishukuru sana
serikali kwa niaba ya wananchi wa jimbo kwa kuunganisha mkoa wa Simiyu na
Shinyanga kupitia jimbo la Maswa Magharibi. Barabara ya Mwigumbi mpaka Maswa
kwa sasa tayari imekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami. Faida za barabara
hii pamoja na kuunganisha mkoa na mikoa mingine, lakini pia wananchi wa jimbo
la Maswa Magharibi wataweza kupata masoko ya mazao yao na huduma zingine kwa
urahisi Zaidi kwa sasa kulinganisha na huko nyuma. Mbunge wa jimbo anayo
matumaini makubwa kwamba barabara ya kutoka Ikungu/Njiapanda kwenda Malampaka
pia itamalizika kujengwa kwa wakati kwa kiwango cha lami kwa sababu tayari
mwaka wa fedha 2018/2019 ilipangiwa bajeti ya Tshs milioni 800 na mwaka huu wa
fedha 2019/2020 pia imepangiwa bajeti ya Tshs milioni 300. Tayari mkandarasi wa
kujenga barabara hii ameshaanza kazi ya ujenzi.
5.
KILIMO
NA UZALISHAJI:
Pamoja na kuisimamia serikali ngazi ya
wilaya mpaka taifa, ofisi ya mbunge imeweza pia kuhamasisha wakulima ndani ya
jimbo kulima na kuzalisha mazao kwa tija kubwa ili kujipatia mazao mengi na
hivyo kujiongezea kipato hatimaye. Kwa kushirikiana na tume ya umwagiliaji ya
kanda na wilaya mradi wa mtaro wa umwagiliaji wa Kinamwigulu umekamilika.
Mheshimiwa mbunge kwa kushirikiana na Shirika la World Vision waliweza
kukamilisha mradi wa umwagiliaji wa Masela kwenye kitongoji cha Isebya. Vijana
wa kikundi cha kijiji cha Gumali walipatiwa msaada wa pampu ya umwagiliaji na
mifuko 10 ya siment ili waweze kukarabati mtaro wao wa maji unaotumika kupeleka
maji kwenye majaruba ya mpunga na bustani zao ambazo hulima majira yote.
Kikundi kimojawapo cha kijiji cha
Gumali kinachojishughulisha na kulima bustani.
Tumeweza kuisimamia vizuri serikali na
hivyo kuwa na bei inayomlipa mkulima kwenye zao la pamba. Mfano mwaka wa fedha
2014/15 bei ya pamba ilikuwa Tshs 800, mwaka wa fedha 2015/16 bei ya pamba
ilipanda kufikia Tshs 1000, mwaka wa fedha 2016/17 bei ilikuwa 1200, mwaka wa
2017/18 bei ilikuwa Tshs 1100, na mwaka wa fedha 2018/19 bei ni Tshs 1200.
Kutoshuka kwa bei ya pamba ni matokeo ya usimamizi mzuri wa bunge kwa serikali
kuhakikisha kwamba wakulima hawapunjwi mazao yao wanayozalisha kwa jasho kubwa.
Matokeo yake uzalishaji katika zao la pamba umeongezeka na mwaka huu wa 2019
uzalishaji umeongezeka Zaidi.
6.
VIWANDA
Katika kutimiza adhima ya Tanzania ya
viwanda ifikapo 2025, jimbo limewezeshwa kuanzisha viwanda viwili, kimoja cha
kuongeza viini lishe kwenye unga wa viazi ambacho kimejengwa kijiji cha
Njiapanda.
7.
MINADA
NA MASOKO.
Jimbo lina minada ya ng’ombe mikubwa 2
panapouzwa na kununua nafaka, mifugo, nguo, nk. Minada hiyo ni Malampaka na
Jija. Mwaka 2015 mnada wa Jija ulikuwa na changamoto kiasi kwamba mnada haukuwa
unafanya kazi kwa sababu ya kuzidiwa kete na halmashauri ya wilaya ya Kwimba
walipoanzisha mnada wa Maligisu kinyemela. Mbunge kwa kushirikiana na
halmashauri ya wilaya ya Maswa alifanya juu chini kuufufua mnada huu ikiwa ni
pamoja na kuwasiliana na wizara ya mifugo makao makuu na hatimaye mnada huo
ulianza tena kufanya kazi mwaka 2017. Katika minada hii pia kulikuwa na kero
mbalimbali kama vile ushuru uliokuwa ukijulikana kama makanyagio. Ushuru huu wa
makanyagio umefutwa na serikali kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na mbunge
akishirikiana na wabunge wengine wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
8.
MICHEZO
NA BURUDANI.
Kwa upande wa michezo na burudani,
tumejitahidi sana kuwaunganisha vijana walioko mashuleni na wasio shuleni kwa
njia ya michezo na burudani. Maeneo mengi tumeweza kutoa mipira ya mguu, mipira
ya pete, jezi na kugharamia kuweka magoli kwenye baadhi ya viwanja vya michezo
hasa vya mpira wa miguu shuleni.
Mheshimiwa mbunge akitoa mpira kwa
moja ya shule ya msingi jimboni.
Mheshimiwa
mbunge alipokuwa mgeni rasmi kwenye mashindano ya ligi ya mkoa wa Simiyu.
Mashindano yalifanyika wilaya ya Maswa uwanja wa CCM.
Mheshimiwa
mbunge wakati alipotoa zawadi kwa washindi ligi ya mpira wa miguu iliyofanyika
shishiyu sekondari.
MWISHO.










Comments
Post a Comment