MJUE MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA MASWA MAGHARIBI.



Ndugu MASHIMBA  MASHAURI NDAKI alizaliwa tarehe 7/12/1962 katika kijiji cha Jihu Kata ya Badi wilaya ya Maswa. Alisoma shule ya Msingi Isanga iliyoko kata ya Isanga mwaka 1972-1978. Alijiunga na shule ya sekondari ya Buluba mwaka 1980 na kumaliza kidato cha nne mwaka 1983, ambapo mwaka 1984 mpaka 1986 alichaguliwa kujiunga na kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya wavulana Songea. Mwaka 1986/87 alijiunga na jeshi la kujenga taifa kwenye kambi ya Bulombora iliyoko mkoani Kigoma ambapo alihitimu mafunzo ya kijeshi kwa mwaka mmoja.
Ndugu NDAKI mwaka 1988 mpaka 1992 alianza kusoma na kuhitimu shahada (digrii) ya uchumi katika chuo kikuu cha Dar-es-Salaam. Mwaka 2001 mpaka 2003 alirudi tena shuleni na kusoma na kisha kuhitimu shahada (ya pili) ya uzamili ya mambo ya uchumi jamii ya chuo kikuu cha Southern New Hampshire cha Marekani.  

INAENDELEA..............

KAZI.
Mara baada ya kuhitimu masomo yote hayo ndugu NDAKI alifanya kazi ya kufundisha somo la Uchumi Buluba High School kwa miaka miwili Mei, 1993 mpaka Agosti, 1995. Septemba 1995 alijiunga kufanya kazi na Shirika la Kimataifa la World Vision kwenye miradi ya Uhai wa Mtoto (Child Survival) mradi uliokuwa wilayani Kahama mpaka mwaka 1999.
Hatimaye Januari 2000 Shirika kwa kuzingatia utendaji wake wa kazi alipandishwa cheo na kupewa kazi ya Uratibu wa ufuatiliaji na tathimini na kuhamishiwa  Kanda ya Ziwa iliyokuwa na makao yake mjini Shinyanga.Alifanya kazi hiyo mpaka Aprili 2005. Mnamo Mei 2005, kwa kuzingatia pia uadilifu, uaminifu na utendaji kazi wake, Shirika la World Vision lilimpandisha tena cheo na kuwa Meneja wa Kanda na kumhamishia Kanda ya Kaskazini yenye makao yake mjini Arusha. Aprili 2008 Ndugu NDAKI alihamishiwa na shirika kwenda Kanda ya Ziwa ambapo anaendelea akiwa Meneja wa Kanda. Mwaka 2011 Oktoba, ndugu NDAKI alipandishwa tena cheo na kuwa Mkurugenzi Mshiriki wa miradi kazi ambayo anafanya mpaka wakati huu. Baada ya kufanya kazi na jamii kwa uadilifu na uaminifu kwa miaka 20 sasa, Ndugu NDAKI anaomba ridhaa ya wanachama wa CCM ili kuwatumikia wananchi wa Maswa Magharibi kwa nafasi ya UBUNGE.


DHAMIRA.
Kazi ya ubunge ni kazi ya uongozi, na kuongoza ni kuonyesha njia,hivyo kwa kutumia utashi, akili, ujasiri, usikivu, utii, elimu na vipaji alivyopewa na Mwenyezi Mungu ndugu NDAKI atashirikiana na wakazi wote wa Jimbo la Maswa Magharibi, serikali na wadau wengine wa maendeleo,  ili kujiletea maendeleo zaidi na kutatua kero mbalimbali zinazotukabili kwa kuzingatia ilani ya uchaguzi ya CCM na sera za serikali yake.
Mkazo mkubwa katika kutimiza azima hii utakuwa ni:- 

> kuboresha/kupandisha elimu kwa ujumla kwenye jimbo kwa kuboresha miundo mbinu yake na kuwezesha kupatikana kwa vifaa mbalimbali pamoja na vitabu kwa shule za Msingi na Sekondari. Sote tunajua umuhimu wa elimu katika jamii yoyote ile.
>  Kuboresha huduma za afya kwa watu wote hasa akina mama na watoto. Tutaweka nguvu kwenye utoaji wa huduma zenyewe.

> Mkazo pia utawekwa kwenye swala la kuongeza kipato cha kaya kwa kutumia mbinu ya kuunganisha nguvu zetu katika vikundi vya wazalishaji mali.   Vijana kati ya umri wa miaka 18 na kuendelea, wafugaji, wakulima na akina mama watahamasishwa kuwa katika vikundi vya uzalishaji mali na kupatiwa mafunzo husika kwa muda mfupi na mrefu ili waweze kuendesha shughuli zao kitaalamu. Maji ni muhimu kwa binadamu na  mifugo yetu. Mkazo pia utawekwa kwenye swala hili. 
Yote haya yanawezekana kwa kushirikiana nakwa kuchagua MBUNGE/MWAKILISHI  makini, sahihi, mbunifu na mahiri katika kushirikisha wananchi,  kwa kuwa pamoja nao kuweka Vipaumbele nao, na kufanya nao. Ndugu NDAKI ni chaguo lako sahihi. Kwa pamoja maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana.


“KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI”


MGOMBEA UBUNGE WA JIMBO LA MASWA MAGHARIBI
 
                                                  NDUGU                      
                                               MASHIMBA M.  NDAKI          




 

Comments