Kinana: Wanaoona Misingi ya CCM haifai Waondoke.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana ameendelea kusisitiza kuwa chama kinarudishwa kwenye misingi yake akitaka mtu anayefikiri misingi hiyo haifai, aondoke atafute mahala pengine.
 
Kinana ambaye katika ziara zake tangu akiwa Kagera, Geita na sasa Mwanza, amekuwa akisisitiza viongozi wa CCM kuhudumia wananchi na kuwatendea haki, alisema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara mjini Sengerema.
 
“Nataka niwahakikishe watanzania tunakirudisha hiki chama kwenye misingi. Na kama kuna mtu anafikiri misingi hiyo haifai, bora aondoke kwenye CCM atafute mahala pengine pa kwenda,” alisema.
 
Akishangiliwa na umati wa watu uliohudhuria mkutano huo, Kinana aliwataka wanasiasa kushikamana kusemea wanyonge. Alisema watu wengi hawana vyama vya siasa isipokuwa wanalazimika kuingia kutafuta maisha.
 
Katibu Mkuu alisema wanachotaka ni kuhakikisha chama kinakuwa karibu na watu, kinawasikiliza na kuwasemea.
 
“Hiki ndicho chama tunachokijua sisi wengine,” alisema na kusihi wana CCM kushikamana katika kusimamia misingi ya watu kwa kupinga mambo ya hovyo na kuunga mkono mambo mazuri.
 
Alisema mtu anayekiri upungufu wake si mtu dhaifu bali ni imara. Alisema si kila jambo linapawa kukubaliwa.
 
“Watu wananyimwa haki yao, sawa, wanadhulumiwa, tuko mbioni,...nataka niwahakikishie watanzania, tunakirudisha hiki chama kwenye misingi,” alisisitiza.
 
Alisema kazi ya serikali ni kutengeneza mazingira, watu wapate mahitaji yao. Pia alisema serikali inapaswa kusimamia sheria.

Dkt. Nchimbi Atangaza Rasmi Kutogombea Ubunge Songea


  Katika hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya wananchi wakiwemo wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, wamejikuta katika hali ya sintofahamu huku wengine wakimwaga machozi baada ya mbunge wa jimbo hilo, mh. Dkt. Emmanuel Nchimbi kutangaza rasmi kutogombea tena ubunge katika jimbo hilo.


Nchimbi aliyelitumikia jimbo hilo kwa miaka 10 alikutana na wanachama wa chama cha mapinduzi Katika uwanja  wa majimaji mjini Songea pamoja na kuelezea mafanikio mbalimbali ya maendeleo aliyoyafanya katika jimbo hilo ikiwemo ujenzi wa barabara, zahanati na shule za sekondari lakini pia akatumia nafasi hiyo kutangaza rasmi kutogombea tena ubunge katika jimbo la songea mjini.

Tamko hilo la dkt. Nchimbi lilizua simanzi kwa baadhi ya wananchi na wanachama wa CCM  Songea huku wengine wakishindwa kujizuia na kujikuta wakimwaga machozi.

Katika maelezo yao wanachama hawa walisema kuachia ngazi kwa Dkt, Nchimbi kutogombea katika jimbo hilo kunatoa fursa kubwa kwa vyama vya upinzani kuchukua jimbo hilo hali ambayo hawakubaliani nayo.

Hata hivyo wanachama hao walimuomba mbunge huyo kutengua msimamo wake na kumtaka arejee tena kugombea jimbo la Songea mjini, jibu la dkt. Nchimbi likawa anaenda kufikiria.

Comments